Msigwa amesema ingawa kwa sasa yupo kwenye kampeni ya Uchaguzi Mkuu lakini anatenga muda wa kufuatilia mechi zetu huku matumaini juu yetu yakiwa ni makubwa kutokana na ubora wa timu tuliyonayo.
Msigwa ameyasema hayo wakati wa kukabidhi kitita cha Shilingi milioni 15 kwa timu kama zawadi ya bao la mama kufuatia ushindi wa mabao 3-0 tuliopata dhidi ya Nsingizini Hotspurs katika mchezo wa hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Jumapili iliyopita.
"Rais Dkt. Samia amenikabidhi kiasi hiki cha pesa ili niwaletee baada ya ushindi mliopata wiki iliyopita. Kiukweli Rais anawaamini sana na ana matumaini nanyi makubwa ya kuzidi kufanya vizuri," amesema Mh. Msigwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Crescentius Magori ameweka wazi kuwa malengo ya klabu ni kuhakikisha tunazidi kufanya vizuri ikiwezekana kufika mpaka fainali.
Nae nahodha wa timu, Shomari Kapombe akizungumza kwa niaba ya wachezaji amesema kiasi hicho cha pesa wanachopata kutoka kwa Rais Samia, ni motisha ya kuendelea kupambana ili kufikia malengo tuliyojiwekea.
"Hii ina maana kubwa kwetu, na tunamshukuru Mh. Rais kwa motisha anayotupa na mimi nichukue nafasi hii kumuahidi kuwa hatutamuangusha," amesema Kapombe.