Matola amesema wachezaji wameandaliwa kimbinu na kisaikolojia kutokana na wapinzani tutakaokutana nao kwakuwa malengo yetu ni kushinda na kupata pointi tatu.
Matola ameongeza kuwa pamoja na upinzani ambao tunategemea kukutana nao lakini tupo tayari kuwakabili na tutaingia uwanjani kwa kutafuta mabao mengi huku tukijilinda vema tusiruhusu bao.
Akizungumzia hali ya kikosi, Matola amesema mchezaji pekee ambaye hatakuwa sehemu ya mchezo kutokana na majeruhi ni mlinda mlango Moussa Camara huku wengine wote wakiwa tayari kuipambia timu.
"Tunafahamu itakuwa mechi ngumu, tunategemea kupata upinzani mkubwa kutoka kwa JKT, haijawahi kuwa mechi nyepesi kila tunapokutana lakini tupo tayari."
"Jambo la kumshukuru Mungu ni kwamba wachezaji wote wapo tayari kwa mchezo isipokuwa Moussa Camara ambaye bado anaendelea na matibabu," amesema Matola.
Akizungumzia kwa niaba ya wachezaji mlinzi wa kati, Wilson Nangu amesema wapo tayari kufuata maelekezo watakayopewa na walimu na kupambana muda wote wa mchezo ili kuisadia timu kupata alama tatu.
"Tunawaheshimu JKT lakini tupo tayari kuwakabili. Nitafurahi kucheza katika ardhi niliyoizoea lakini safari hii nitakuwa naisaidia timu yangu ya Simba kupata ushindi," amesema Nangu.