Kapombe aliumia mazoezini wiki tatu zilizopita na kukosa mechi zote za kufuzu Ligi Mabingwa Afrika na nyingine za Ligi kuu ya NBC.
Meneja Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally amesema kwa mujibu wa jopo la madktari wetu Shomari alichanika nyama za paja lakini kwa sasa amepona na yuko tayari kuendelea na majukumu yake.
Wakati huo huo, kiungo mkabaji Sadio Kanoute anaendelea vema na sasa ameanza mazoezi binafsi ya gym ili kuweka mwili sawa.
Kanoute aliugua tonsils 'mafindofindo' siku chache kabla ya mchezo wetu dhidi ya Yanga hivyo kuondolewa kikosini kufuatia homa kali iliyokuwa inamkabili.
Kwa sasa Kanoute amepona na ameanza mazoezi mepesi lakini bado hajawa tayari kwa mchezo wa Alhamisi dhidi ya Azam maarufu Mzizima Derby.
Ahmed ameongeza kuwa mlinzi wa kulia Israel Patrick ataukosa mchezo dhidi ya Azam baada ya kupata majeraha katika mchezo uliopita dhidi ya Yanga na tayari ameshafanyiwa vipimo na huenda akakaa nje ya uwanja kwa wiki mbili.
"Kapombe amerejea na amefanya mazoezi na wenzie na mwalimu akiona inafaa anaweza kumtumia dhidi ya Azam, Sadio yeye anaendelea vizuri na anafanya mazoezi ya Gym lakini Israel hatakuwa sehemu ya mchezo baada ya kuumia dhidi ya Yanga juzi Jumapili," amesema Ahmed.