Mshambuliaji kinara Medie Kagere, amewaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumapili kuipa sapoti timu kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Orlando Pirates.
Kagere amesema mashabiki ni wachezaji wa 12 uwanjani wana mchango mkubwa kwa timu kufanya vizuri na kupata ushindi hivyo kwa uwepo wao anaamini tuna nafasi kubwa ya kuifunga Orlando Jumapili.
Amesema wakati mwingine wachezaji wanakuwa wamechoka uwanjani lakini zile shamra shamra za mashabiki zinawapa nguvu ya kuendelea kupambana na kupata ushindi.
"Mashabiki ni watu muhimu sana, tunaweza kusema ni wachezaji wa 12 uwanjani. Uwepo wao unatupa nguvu sana kuendelea kupambana kuipatia timu ushindi.
"Hii ni mechi muhimu kwetu, tunapaswa kushinda nyumbani ili iwe rahisi katika mchezo wa marudiano kule Afrika Kusini, kwa hiyo sisi peke yetu hatuwezi tunahitaji sapoti ya mashabiki," amesema Kagere.