Simba Sports Club
News

'Hatumdharau yoyote Mapinduzi Cup'

4 Jan 2022

Meneja wa timu Patrick Rweyemamu, amesema tumejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri katika Michuano ya Kombe la Mapinduzi na hatutaidharau timu yoyote mechi zote zitakuwa kama fainali.

Rweyemamu amesema sababu ya kuja na kikosi kizima ni kuhakikisha tunatimiza malengo yetu ya kutwaa ubingwa wa michuano hiyo baada ya kupita muda mrefu.

Akizungumzia mchezo wa kesho dhidi ya Selem View, Rweyemamu amesema tunaamini utakuwa mgumu na tupo tayari kupambana kwa ajili ya kupata alama zote tatu.

"Tumekuja Zanzibar na kikosi cha wachezaji 26 tuliowasajili msimu huu. Kuna wengine wawili wamekuja kwa majaribio kwa hiyo wapo 28, hii inaonyesha wazi tumedhamiria kufanya vizuri.

Advertisement

"Katika wachezaji 28 ni wawili tu Taddeo Lwanga na Erasto Nyoni ambao hawatakuwa sehemu ya mchezo sababu bado wapo chini ya uangalizi wa daktari lakini waliobaki wapo kamili kupigania alama tatu," amesema Rweyemamu.

Kwa upande wake mlinzi wa kushoto, Gadiel Michael amesema morali za wachezaji zipo juu na kila mmoja yupo tayari kwa mchezo wa kesho lengo ni kupata ushindi kwenye mechi ya ufunguzi.

"Wachezaji wote tupo tayari kwa ajili ya mchezo wa kesho, kila atakayepata nafasi ya kucheza atapambana kuhakikisha tunapata ushindi," amesema Gadiel.

Back to homepage
Share this story