Kiraka Erasto Nyoni amewataka mashabiki wetu kujitokeza kwa wingi Jumamosi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga ili kuongeza hamasa na kusaidia kupatikana kwa ushindi.
Erasto amesema anatamani idadi ya mashabiki waliojitokeza kwenye Tamasha la Simba Day iwe mara mbili Jumamosi na wao kama wachezaji hawatawaangusha.
Nyota huyo ameongeza kuwa mchezo utakuwa mgumu na siku zote mechi ya Derby ipo hivyo lakini kwa maandalizi tuliyofanya anaamini tutaibuka na ushindi mbele ya Yanga.
"Mimi ninachoomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi na ikiwezekana iwe mara mbili ya ilivyokuwa juzi kwenye Tamasha la Simba Day na sisi wachezaji tunaahidi hatutawaangusha."
"Mchezo utakuwa mgumu tunawaheshimu Yanga na mechi ya Derby haijawahi kuwa rahisi lakini tumejipanga kushinda kutokana na maandalizi tuliyofanya na uwezo huo tunao," amesema Erasto.