Kiungo mshambuliaji Hassan Dilunga, ameondoka nchini leo kuelekea Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu ya majeraha yanayomsumbua.
Kutokana na vipimo alivyofanyiwa na madaktari, Dilunga anatakiwa kufanyiwa upasuaji na atakuwa Afrika Kusini kwa muda wa wiki tatu au nne.
Dilunga ambaye amekuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu ameushukuru uongozi wa klabu kwa kughramia matibabu hayo ambapo anaamini atarejea akiwa fiti kuitumikia timu.
"Kwanza naushukuru uongozi wangu kwa kunipeleka Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu ni jambo jema, naamini nitarudi nikiwa fiti kuitumikia timu," amesema Dilunga.
Kuelekea mchezo wetu wa Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Orlando Pirates, Dilunga ameitakia heri timu kufanya vizuri huku akiwaasa wachezaji kujitoa kwa nguvu zote kuhakikisha tunashinda.
Dilunga pia amewaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi na kuujaza uwanja Jumapili ili kuwapa hamasa wachezaji.
"Naitakia heri timu katika mchezo wetu muhimu wa nyumbani dhidi ya Orlando. Nawaomba wachezaji wenzangu wapambane najua Watanzania wako nyuma yao pia mashabiki mnapaswa kwenda uwanjani kwa wingi kuipa sapoti timu ninaamini tutapata ushindi," amesema Dilunga.