Benchikha amesema amekubali kuja kufanya kazi nasi na anaamini ataweza kuirejesha timu katika hali yake ya ushindi.
Akizungumzia hali ya kikosi Benchikha amesema yupo tayari kufanya kazi na yoyote ambaye anajituma na kipindi hiki atakuwa anaangalia mchezaji mmoja mmoja katika kila nafasi.
"Nipo tayari kufanya kazi Simba, ninafahamu timu haipo kwenye hali nzuri kwa sasa lakini naamini kwa pamoja tutaweza kurejesha heshima ya timu.
"Mimi ni mpambanaji na siogopi changamoto nipo hapa kuifanya Simba kuwa timu bora na kutwaa mataji. Tunataka kufanya vizuri katika michuano yote tunayoshiriki," amesema Benchikha.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Klabu, Imani Kajula amesema ujio wa Benchikha na wasaidizi wake unalingana na mahitaji na timu kwa sasa ambao anaamini utarejesha timu kwenye ushindi.
"Haikuwa rahisi kumpata Benchikha, huyu ni kocha wa daraja la juu ametoka kuchukua taji la Shirikisho na Super Cup ndio maana imechukua muda kidogo lakini sisi kama uongozi tuna imani nae," amesema Kajula.