Barker amesema kurejea kwa wachezaji waliokuwa kwenye majukumu ya timu za Taifa kumeongeza nguvu na kumewapa wigo mpana kama benchi la ufundi kufanya uchaguzi wa kikosi kwenye mchezo wa kesho.
Barker ameongeza Simba ni timu kubwa na mara zote inapambana kwa ajili ya ubingwa hivyo ili kutimiza hilo lazima kupata ushindi kwenye kila mchezo na hilo ni moja ya malengo yetu.
Akizungumza hali ya kikosi, Barker amesema tutawakosa wachezaji wawili Jonathan Sowah na Allasane Kante ambao wanatumikia adhabu lakini Morice Abraham aliyekuwa majeruhi amerejea kikosini.
"Tupo tayari kwa mchezo wa kesho, wachezaji wapo hali nzuri na tayari kwa mechi ambayo tunafahamu itakuwa ngumu. Tumejipanga kuhakikisha tunashinda kwakuwa malengo yetu ni kupigania ubingwa," amesema kocha Barker.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji kiungo mkabaji, Daud Semfuko amesema kwa upande wao wapo tayari kuhakikisha wanapambana mpaka mwisho na kufuata maelekezo watakayopewa na walimu ili alama tatu muhimu zipatikane.
"Kwa upande wetu kama wachezaji tupo tayari, kila atakayepata nafasi ya kucheza atakuwa tayari kuipigania timu kupata matokeo na hilo ndilo lengo kuu," amesema Semfuko.