Barker amesema ili kushinda mechi kubwa kama ya kesho unapaswa kucheza kwenye kiwango bora na kupunguza makosa ambayo yanaweza kukugharimu pamoja na kutumia nafasi zitakazopatikana.
Barker ameongeza kuwa wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri na morali zipo juu na anaamini tuna nafasi nzuri ya kupata ushindi kwenye mchezo wa kesho.
"Nimeongea na wachezaji na kuwasisitiza kutokuwa na presha kuelekea mchezo wa kesho kutokana na matokeo ya nyuma tuliyopata dhidi yao badala yake tunapaswa kujiamini."
"Ili kushinda mechi kubwa kama hii tunapaswa kuwa kwenye kiwango bora na kutumia vizuri nafasi tutakazopata. Nafikiri tuna nafasi ya kufanya vizuri," amesema Barker.
Kwa upande wake nahodha, Shomari Kapombe amesema maandalizi yamekamilika kwa asilimia 100 na kila mchezaji yupo tayari kuhakikisha ushindi unapatikana kwenye mchezo wa kesho.
Kapombe ameweka wazi kuwa hatujapata ushindi dhidi yao kwenye mechi kadhaa tulizokutana nao lakini hiyo imebaki kuwa historia na kesho ni siku mpya na tumejipanga kuhakikisha tunashinda.
"Tunajua tuna jukumu zito kuelekea mchezo dhidi ya Yanga kesho kutokana na kupoteza mechi nyingi dhidi yao lakini tumejipanga kuhakikisha tunajirekebisha na kupata alama tatu kwakuwa malengo yetu ni kutwaa ubingwa msimu huu," amesema Kapombe.