Simba Sports Club
News

Banda kuondoka leo kujiunga na The Flames tayari kwa AFCON

4 Jan 2022

Winga wetu Peter Banda, ataondoka leo saa 11 jioni kuelekea Malawi kujiunga na Timu ya Taifa ya Malawi (The Flames) inayojiandaa na Michuano ya AFCON inatakayofanyika nchini Cameroon kuanzia Januari 9.

Banda anakwenda moja kwa moja nchini Cameroon ambapo atakutana na wachezaji wenzake tayari kwa mashindano hayo.

Malawi imepangwa Kundi B pamoja na Timu za Senegal, Zimbabwe na Guinea. The Flames itaanza kutupa karata yake ya kwanza dhidi ya Guinea Januari 10.

Banda amesema anafurahi kushiriki michuano hiyo kwa kuwa atakutana na wachezaji wakubwa wanaofanya vizuri barani Ulaya ambapo atajifunza mengi kutoka kwao.

Advertisement

Banda ameongeza kuwa atahakikisha anafanya vizuri ili kulisaidia taifa lake na kuitangaza Simba kupitia michuano hiyo mikubwa barani Afrika.

"Hii ni michuano mikubwa na kila mchezaji Afrika anatamani kushiriki. Kwangu ni jambo kubwa na nitahakikisha nafanya vizuri kuisaidia nchi yangu na kuitangaza Simba," amesema Banda.

Banda atakutana na nyota wengine watatu wanaocheza Ligi Kuu ya NBC ambao ni Prince Dube, Bruce Kangwa na Never Tigere wa Zimbabwe alio nao kundi moja.

Back to homepage
Share this story