Winga mpya wa kikosi chetu Peter Banda, amefunguka kuwa baada ya mazoezi ya leo Nahodha John Bocco alimfuata na kumwambia atulize akili acheze mpira kwa sababu Wanasimba wana matumaini makubwa juu yake.
Raia huyo wa Malawi ni miongoni mwa nyota wetu wapya ambao tayari wameanza kuonyesha wana kitu kikubwa miguuni na wanatakiwa kupewa muda.
Banda amesema kitendo cha Bocco kumfuata na kuongea naye, kumemuongezea motisha na hali ya kujiamini na anaamini kila kitu kitakaa sawa na ushindi utapatikana.
"Nahodha alikuja kuongea nami na kikubwa ameniambia niendelee kujituma na kutuliza akili kwa kuwa timu inanihitaji na kwangu hilo ni jambo kubwa na linanifanya niongeze jitihada kila nitakapopata nafasi ya kucheza," amesema.
Akizungumzia mchezo wa kesho dhidi ya Dodoma Jiji, Banda amesema hakuna chochote kinachohitajika zaidi ya ushindi na wao kama wachezaji watajitahidi kuhakikisha hilo linafanikiwa na kuwapa mashabiki furaha.
"Tunahitaji kushinda kwenye mchezo wa kesho ni muhimu kwetu na wachezaji tunalijua hilo tutapambana hadi mwisho kuhakikisha tunawapa mashabiki wetu furaha," amesema Banda.