Matola amesema tunategemea kupata upinzani mkubwa kutoka kwa Namungo kutokana na ubora walionao lakini hata hivyo tupo tayari kuhakikisha tunapata alama tatu.
Kuelekea mchezo huo Matola amesema kikosi kipo tayari isipokuwa tutaendelea kuwakosa Mohamed Bajaber na Abdulazak Hamza ambao bado ni majeruhi.
"Tupo tayari kuhakikisha tunapata alama zote tatu kwenye mchezo wa nyumbani, tunafahamu itakuwa mechi ngumu na mara zote tunapokutana na Namungo ushindani unakuwa mkubwa."
"Kuhusu hali ya kikosi, tunamshukuru Mungu wachezaji wapo kwenye hali nzuri na leo jioni tutafanya mazoezi ya mwisho ingawa tutaendelea kuwakosa Bajaber na Hamza ambao bado ni majeruhi," amesema Matola.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji mlinzi wa kushoto, Anthony Mligo amesema maandalizi ya mchezo yamekamilika na tupo tayari kuhakikisha ushindi unapatikana.
Mligo ambaye msimu uliopita alikuwa akiitumikia Namungo amekiri kuwa utakuwa mchezo mgumu kwakuwa mara zote wanapocheza mechi kubwa wanakuwa na morali ya hali ya juu.
"Tunafahamu itakuwa mechi ngumu, Namungo ni timu imara lakini tumejipanga kuhakikisha tunapata ushindi katika mchezo wetu wa nyumbani," amesema Mligo.