Ahmed ameyasema hayo wakati akiongea na Wanasimba wa Mkwajuni Visiwani Zanzibar kuelekea mchezo wetu wa nusu fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo amewaomba wahakikishe wanafanya kila linalowezekana timu ipate matokeo chanya.
“Kwa mara ya kwanza Simba inacheza mchezo wa kimataifa kwenye ardhi ya Zanzibar, tumebakiwa na dakika 180 za kwenda fainali, 90 za kwanza hapa Zanzibar na 90 zingine itakuwa Afrika Kusini. Sasa 90 ndio za thamani zaidi inatakiwa tumalize kazi tukiwa hapa," amesema Ahmed.
Ahmed ameendelea kusema kuwa "Mechi hii ni mechi yenu watu wa Zanzibar na hili tunaamini mnaliweza. Mimi naamini hii inawezekana na mzigo huu Wazanzibar mnaumudu na kuipeleka Simba fainali.”
“Niwambie Wanasimba wote popote walipo kwenye ardhi hii ya Tanzania popote sisi tunafika. Simba ni ya watu wote na sehemu yoyote tutafika ilimradi ni kwa Wanasimba wenzetu. Niseme kwamba tarehe 20 tuna kazi kubwa tunatakiwa kuikamilisha kwenye Uwanja wa Amaan," amesema Ahmed.
Ahmed ameongeza kwa kusema ushindi ambao tunauhitaji ni kuanzia mabao matatu na hili linawezekana kwa aina ya maandalizi tuliyonayo na nguvu kubwa ni kutoka kwenu Wazanzibari.