Akizungumza na wanachama, mashabiki na wapenzi waliojitokeza kwenye tukio hilo Ahmed amekiri kuwa amefurahishwa kuongezeka kwa familia ya Wanasimba huku akiwaomba wengine ambao tayari wamejikusanya kufuata taratibu ili watambuliwe kama ilivyo kwa Wekundu wa Kurasini Mji mpya.
“Ninayo furaha kubwa kwa kufanikisha uzinduzi wa tawi hili kwa kushirikiana na viongozi wengine, ni rasmi sasa kwamba Wekundu wa Kurasini Mji Mpya ni tawi la Simba Sports Club, tunayo furaha kuongeza mtoto kwenye familia ya Simba.”
“Pamoja na kwamba tuko hapa kwa uzinduzi wa tawi na rasmi linaanza kufanya kazi za Simba. Kuzindua tawi ni jambo moja tena jambo jepesi, jambo gumu linalofata sasa ni kulitunza na kulisimamisha kuwa na ustawi bora," amesema Ahmed.
Baada ya uzinduzi huo Ahmed amewaomba wanachama hao kuhakikisha wanajitoa kwa asilimia 100 katika masuala ya maendeleo ya klabu ikiwemo kujitokeza uwanjani wakianza na mechi ya kesho ya Ligi Kuu dhidi ya Mashujaa na ile ya Jumapili ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya ES Tunis.
“Yapo mawili wiki hii na tunatakiwa kuyafanya kwa ukamilifu wa asimilia 100. Moja lipo kesho, mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mashujaa FC. Ushindi wa kesho ni muhimu kwanza tutapata mazoezi ya maana kujiandaa na ES Tunis, matokeo mazuri katika mchezo huu yana faida kwetu kwenye kuamsha morali kuelekea mechi ya Februari Mosi siku ya Jumapili," amesema Ahmed.