Kauli ya Robertinho kuelekea mchezo wa Kesho dhidi ya Vipers

Kocha Mkuu, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema tumepata wiki moja maandalizi ya mchezo wetu wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vipers utakaopigwa Kesho Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Robertinho amesema kitu kizuri kinachomfurahisha ni jinsi hali ya kujiamini kwa wachezaji na wanavyojituma mazoezini.

Robertinho ameongeza kuwa mpaka sasa tayari anacho kikosi cha wachezaji 11 waliofiti ambao wataanza kwenye mchezo wa kesho.

“Mimi ni mtu chanya siku zote, nina muamini Mungu, nawaamini wachezaji wangu, nina miezi mitatu tangu niwe hapa lakini tumeanza kubadilika kiuchezaji.

“Vipers ni timu nzuri, inacheza soka la kushambulia kwa kushtukiza, tumefanya maandalizi ya kuwadhibiti ili tupate ushindi. Ninaamini hatua kwa hatua tunaweza kuvuka na kuingia robo fainali,” amesema Robertinho.

Kwa niaba ya wachezaji, mlinzi wa kulia Shomari Kapombe amesema wamejipanga kuhakikisha wanarudisha heshima ya Uwanja wa Benjamin Mkapa baada ya kupoteza mchezo uliopita.

“Tumeanza vibaya mashindano haya msimu huu lakini wachezaji tumejiandaa, tunajua tuna jukumu zito, tunaenda kucheza kwa kutafuta pointi tatu lakini tunachukua tahadhari kwakuwa Vipers ni timu bora.

“Hatuna presha sababu ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Raja, tumeandaliwa vizuri kimwili na kiakili na tuna imani tutarudisha heshima kwa kushinda, tupo tayari kupambana kwa ajili ya kupata pointi tatu,” amesema Kapombe.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER