‘Wanasimba tukutane kwa Mkapa kusherehekea ubingwa’

Leo tutakabidhiwa taji la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Msimu wa 2020/21 baada ya mchezo wetu dhidi ya Namungo FC utakaopigwa saa 10 jioni Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kutokana na hatua hiyo, tunawaomba mashabiki wetu kujitokeza kwa wingi kushuhudia sherehe za ubingwa na kufunga pazia la Ligi Kuu Msimu wa 2020/21.

Kuelekea mchezo wa leo Kocha Msaidizi, Seleman Matola amesema watapanga kikosi kamili sababu tunahitaji kupata ushindi ili kunogesha shamra shamra za ubingwa.

Matola amesema katika misimu miwili iliyopita hatukuweza kupata ushindi kwenye mchezo ambao tulikabidhiwa ubingwa uwanjani kitu ambacho hatutaki kitokee leo.

“Tumejipanga kuhakikisha tunashinda leo, inapendeza kukabidhiwa ubingwa baada ya ushindi. Namungo ni timu nzuri ila tumejipanga kushinda ili kunogesha shamra shamra za ubingwa.

“Kikubwa mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi na ndiyo maana tutapanga kikosi kamili kile tulichokitumia msimu mzima sababu tumepanga kuwapa raha,” amesema Matola.

TAARIFA YA KIKOSI

Kikosi kipo kwenye hali nzuri wachezaji wapo tayari.

MECHI YA MWISHO TULIPOKUTANA

Tulipokutana katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi, Mei 29 tuliibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Mabao hayo yalifungwa na Chris Mugalu, John Bocco na Bernard Morrison ambaye alifunga kwa mpira alioupiga kutoka katikati ya uwanja na kutinga wavuni moja kwa moja.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER