Tumefanikiwa kupata pointi tatu muhimu katika uwanja wa nyumbani baada ya kuifunga RS Berkane kutoka Morocco bao moja katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi.
Tulianza mchezo kwa kasi na kuliandama lango la Berkane ili tupate bao la mapema la kuwatoa mchezo wapinzani ingawa tulikosa umakini katika umaliziaji.
Pape Sakho alitupatia bao pekee dakika ya 44 baada ya kuwapiga chenga walinzi wa Berkane na kuachia shuti la chini chini lililomshinda mlinda mlango.
Kipindi cha pili tuliongeza kasi kwa kuliandama lango la Berkane huku tukitengeneza nafasi nyingi ambazo hata hivyo hatukuzitumia vizuri.
Hata hivyo, mchezo ulilazimika kusimama kwa takribani dakika tano baada ya ofisa mmoja wa Berkane kuingia uwanjani kushinikiza maamuzi ya mwamuzi.
Kocha Pablo Franco aliwatoa Kibu Denis, Sakho, Rally Bwalya, Medie Kagere na Jonas Mkude kuwaingiza Bernard Morrison, Peter Banda, Mzamiru Yassin, Chris Mugalu na Taddeo Lwanga.
Ushindi huu unatufanya kufikisha pointi saba baada ya kucheza mechi nne tukishinda mbili sare moja na kupoteza moja huku tukisalia na michezo miwili.
One Response