Klabu yetu imeteuliwa kuwa miongoni mwa timu 12 zinazowania kushiriki mashindano mapya ya klabu bingwa ya dunia yatakayofanyika Nchini Marekani mwaka 2025.
Kwa mujibu wa Shirikisho la soka Ulimwenguni (FIFA), Simba ni timu ya namba saba kwa ubora barani Afrika ikiwa na alama 45 hivyo kuwa miongoni mwa timu zinazokidhi vigezo vya kuwania kushiriki kombe hilo.
Ili kushiriki Kombe hilo tunapaswa kuongeza pointi zetu kutoka 45 tulizonazo hadi kufika 81 ambazo wanazo Mamelodi Sundowns wanaoshika nafasi ya tatu au kuchukua ubingwa wa Afrika msimu huu.
Simba ndiyo timu pekee kutoka Tanzania na Afrika Mashariki kuteuliwa kushiriki kombe hilo kutokana na mafanikio yake kwenye michuano ya Afrika.
Mashindano hayo yatajulikana kwa jina la Mundial de Club FIFA ambapo mpaka sasa timu mbili kutoka Afrika zimeshafuzu moja kwa moja ambazo ni Al Ahly na Wydad Casablanca kutokana kuchukua ubingwa hivi karibuni.
Mshiriki mwingine wa kombe hilo ni timu itakayochukua ubingwa wa Afrika msimu huu pamoja na timu itakayokua na alama nyingi zaidi.