Kiasi chote kitakachopatikana katika Kampeni ya Nani Zaidi iliyozinduliwa leo kitatumika katika ujenzi wa miundombinu ya uwanja wetu tutakaoutumia kwenye michuano mbalimbali ya ndani na Kimataifa.
Kampeni hiyo imbayo itahusisha mashabiki wa timu yetu na watani zetu Yanga kupiga kura kushindania ubora timu, jezi na wachezaji ambapo kila moja gharama yake itakuwa Sh 1,000 kupitia mitandao ya simu ya TigoPesa, M Pesa na Airtel Mone
Azam TV na Azam Pay watasimamia zoezi hilo kwa uwazi ambapo matokeo ya kila siku yatatangazwa katika kipindi cha Mshike Mshike Viwanjani kinachorushwa kila siku saa tatu usiku.
Mtendaji Mkuu wa klabu, Barbara Gonzalez amesema kiasi chote cha pesa kitatumika katika ujenzi wa uwanja kutokana na malengo tuliyojiwekea.
“Mwaka jana nilisafiri kwenda Doha, Qatar kwa ajili kujifunza jinsi wenzetu wanavyofanya. Aprili mwaka huu Mwenyekiti, Murtaza Mangungu naye alikwenda Uturuki lengo likiwa ni hilo hilo la ujenzi wa uwanja.
“Sisi kama Simba hii ni hatua ya pili ndiyo maana nasema hela yote itakayopatikana tutajenga uwanja. Baada ya kumalizika kwa msimu kila kitu kitawekwa wazi na bahati nzuri Azam TV itakuwa inatoa maendeleo ya kampeni hii kila siku,” amesema Barbara.
Kwa upande wake Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu, Ahmed Ally amewaomba wanachama, wapenzi na mashabiki kuiunga mkono kampeni hii ili kuweka historia ya kukamilisha malengo tuliyojiwekea.