Tuko Kaitaba leo kuikabili Kagera Sugar

Kikosi chetu leo kitashuka katika Uwanja wa Kaitaba kuikabili Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC saa utakaopigwa moja usiku.

Maandalizi ya mchezo yamekamilika, kikosi kiliwasili juzi hapa Kagera na jana kimefanya mazoezi ya mwisho katika Uwanja wa Kaitaba kujiweka sawa kabla ya mechi ya leo.

Tutaingia katika mchezo wa leo kwa kuiheshimu Kagera na tunajua ni timu nzuri inacheza nyumbani kwa hiyo tumechukua tahadhari zote na lengo ni kuhakikisha tunapata pointi zote tatu.

KAULI YA KOCHA MGUNDA

Kocha mkuu Juma Mgunda amesema wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri na hakuna ambaye atakosekana kutokana na kupata majeraha katika mazoezi ya mwisho jana.

Mgunda ameongeza kuwa mchezo utakuwa mgumu na tunategemea kupata upinzani mkubwa kutoka kwa Kagera lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda na kuondoka na alama zote tatu.

“Tunamshukuru Mungu tumefika salama hapa Kagera, maandalizi yamekamilika na wachezaji wapo kwenye hali, tunategemea kupata upinzani mkubwa lakini tupo tayari kwa mchezo,” amesema Mgunda.

KAPAMA AFUNGUKA KWA NIABA YA WACHEZAJI

Kiungo mkabaji Nassor Kapama amesema morali ya wachezaji ipo na lengo la kila mmoja ni kuhakikisha anapambana kwa jasho na damu kutafuta alama tatu.

Kapama ambaye tumemsajili kutoka Kagera msimu uliopita amesema anaifahamu vizuri timu hiyo na anajua itakuwa mechi ngumu hasa kwa kuwa inachezwa katika Uwanja wa Kaitaba.

“Tunajua mchezo utakuwa mgumu, Kagera ni timu nzuri na ipo nyumbani Kaitaba lakini tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunashinda,” amesema Kapama.

TULIWAFUNGA 2-0 KWA MKAPA

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Agosti 20 tuliibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Mabao yetu yalifungwa kila kipindi ambapo Moses Phiri alifunga kipundi chwa kwanza kwa kichwa na Dejan Georgijevic alifunga la pili.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER