Timu yaingia kambini Kujiandaa na Yanga

Kikosi chetu kimeingia kambini leo asubuhi tayari kwa maandalizi ya mchezo wetu wa Derby dhidi ya watani Yanga utakaopigwa Jumapili, Aprili 16 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa saa 11 jioni.

Kikosi kimerudi jana usiku kutoka jijini Mbeya baada ya ushindi wa mabao 2-0 tuliopata dhidi ya Ihefu FC juzi Jumatatu.

Meneja Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally amesema wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri na hakuna yoyote ambaye tutamkosa kutokana na majeruhi au adhabu ya kadi.

Ahmed amesema mlinda mlango namba moja, Aishi Manula ambaye aliumia bega na mlinzi wa kati Henock Inonga ambao wameukosa mchezo uliopita dhidi ya Ihefu nao wamepona na wapo tayari kwa Derby ya Jumapili.

“Kikosi kimeingia kambini asubuhi na jioni kitaanza mazoezi kujiandaa na mchezo wa Jumapili dhidi ya Yanga. Wachezaji wote wameingia kambini hata wale waliokuwa majeruhi Aishi na Henock,” amesema Ahmed.

Akizungumzia kuhusu kiungo mkabaji, Sadio Kanoute ambaye hakuonekana katika mechi tatu za mwisho zilizopita Ahmed amesema nyota huyo haumwi popote na ameingia kambini tayari kwa Jumapili.

“Kanoute haumwi popote, hakuonekana kwenye mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Raja Casablanca, hakuonekana katika mchezo wa Robo Fainali dhidi ya Ihefu na wa Ligi pia lakini yupo fiti na yupo tayari kwa Jumapili,” amesema Ahmed.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER