Ingawa wengi wanaona ilikuwa kazi nyepesi kuifunga Horoya mabao 7-0 katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Horoya kutoka Guinea, Kocha mkuu Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesema haikuwa rahisi.
Robertinho amesema tuliwandaa wachezaji wetu kucheza vizuri tukiwa hatuna mpira kwakuwa inapunguza kufanya makosa na kuwasoma wapinzani ambapo kunakuwezesha kutumia vizuri nafasi unazopata.
Robertinho ameongeza kuwa malengo yetu yalikuwa kucheza vizuri, kupunguza makosa na kupata ushindi kitu ambacho tumefanikiwa.
“Kupata ushindi mnono wa mabao 7-0 katika Ligi ya Mabingwa sio jambo jepesi na wala haitokei mara kwa mara. Sisi tuliwasisitiza wachezaji wetu kuhakikisha tunacheza vizuri tukiwa hatuna mpira.
“Nawapongeza wachezaji wangu kwa kuweza kufuata maelekezo tuliyowapa na kusababisha kupata ushindi huu, pia nawashukuru mashabiki wetu kwa kujitokeza kwa wingi uwanjani kuipa sapoti timu.”
“Malengo yetu yalikuwa kuingia robo fainali na tunamshukuru Mungu tumefanikiwa hilo ndio jambo zuri la kujivunia,” amesema Robertinho.