Baada ya kufanya mazoezi na kikosi kwa siku mbili katika kambi tuliyoweka nchini Dubai Kocha Mkuu Oliveira Roberto ‘Robertinho’ amejiridhisha kuwa anahitaji mshambuliaji mwingine.
Robertinho amesema kikosi chake kina washambuliaji wazuri huku akimwagia sifa Nahodha John Bocco lakini ameweka wazi kuwa ili atimize malengo yake anahitaji mshambuliaji mwingine wa kusaidiana na waliopo.
“Aina ya mshambuliaji ninayemtaka ni mwenye nguvu, kasi na maarifa ya kufunga,” amesema Roberthinho baada ya kumaliza mazoezi ya leo asubuhi.
Hii ni siku ya pili kikosi chetu kikiendelea na mazoezi mjini Dubai ambapo jana tulifanya mazoezi mara moja na kuanzia leo timu itafanya mazoezi mara mbili yaani asubuhi na jioni.
Kocha Robertinho anasema ameamua kuongeza muda wa mazoezi ili kupandisha nguvu ya timu (Intensity) pamoja na utimamu wa mwili.
Kwa sasa klabu ipo kwenye mawindo ya kutafuta mshambuliaji ili kuongeza ubora kwenye eneo hilo ambapo kabla dirisha dogo halijafungwa mshambualiaji mpya atatangazwa.