Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohamed Dewji 'Mo' leo ameweka Sh bilioni 20 kwa ajili ya uwekezaji baada ya mchakato wa mabadiliko uliodumu kwa miaka minne kukamilika rasmi.
Baada ya Tume ya Taifa ya Ushindani (FCC) kuruhusu mchakato uendelee kutokana na kila kitu kukamilika Mo ameweka kiasi hicho cha fedha kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba yaliyowekwa miaka minne iliyopita.
Mo ameishukuru serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na wote walioshiriki kufanikisha jambo hili kukamilika na Simba inakwenda kuwa kubwa zaidi Afrika.
Mo ameweka wazi kuwa malengo yetu ya baadaye ni kuhakikisha tunakuwa na viwanja nane ikiwamo kikubwa kwa ajili ya timu, timu ya vijana na wanawake ili kushindana na klabu kubwa za Afrika kama Al Ahly, TP Mazembe, Waydad na nyinginezo.
"Nilikuwa nakasirika sana nikisikia watu wakisema eti sina bilioni 20 za kuwekeza Simba. Kwa miaka minne wakati wa mchakato huu nimetumia bilioni 21.3 kwa kusajili, kulipa kambi, Pre Season, maandalizi ya mechi ya Simba na Yanga na mambo mengine lakini hizo hazipo kwenye mkataba.
"Lakini baada ya kila kitu kukamilika leo nimetoa cheki ya bilioni 20 kwa Simba na zile zilizotumika hazihesabiki," amesema Mo Dewji.
Kuhusu usajili Mo ameweka wazi kuwa utakuwa mkubwa msimu ujao na malengo yetu si kuishia robo fainali tena Afrika badala yake tunahitaji kuchukua ubingwa wenyewe.