Kocha Msaidizi, Seleman Matola amesema mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya KMC utakuwa mgumu kutokana na ubora wa wapinzani hao.
Matola amesema mara zote tunapokutana na KMC tunapata upinzani mkubwa lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda.
Matola ameongeza kuwa wachezaji wapo kwenye hali nzuri na kila mmoja yupo tayari kwa mchezo wa kesho.
“Tupo tayari kwa ajili ya mchezo, tunajua itakuwa mechi ngumu na mara zote KMC inatupa upinzani mkubwa lakini tupo tayari kuhakikisha tunashinda.
“Wachezaji walipewa mapumziko ya siku moja baada ya mchezo dhidi ya Wydad Casablanca na baada ya hapo wameendelea na mazoezi na hadi hivi tunavyoongea wapo tayari kwa mchezo,” amesema Matola.
Akizungumzia kwa niaba ya wachezaji mlinzi wa kulia David Kameta ‘Duchu’ amesema pamoja na ugumu ambao tutakutana nao mbele ya KMC lakini tupo tayari kwa mchezo.
“Tupo tayari kwa mchezo na lengo letu ni kuhakikisha tunapambana hadi mwisho ili kupata pointi tatu,” amesema Duchu.