M-bet yabariki ‘Visit Tanzania’ kukaa kifuani CAFCL

Wadhamini Wakuu Kampuni ya Michezo ya Kubashiri ya M-bet imeridhia kuweka neno ‘Visit Tanzania’ kifuani mwa jezi zetu katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambazo tumezizindua leo.

Kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) ikifika hatua ya makundi na kuendelea hakuna nafasi ya kuweka tangazo la mdhamini mwingine kwenye jezi hivyo tumeamua kukaa na M-bet na kuridhia tutumie Visit Tanzania’ kwa ajili ya kuhamasisha Utalii.

Kama ilivyo ada jezi zetu zitakuwa na rangi yetu ile ile ya asili nyekundu kwa nyumbani, nyeupe ugenini na bluu kama neutral.

Mkurugenzi wa Masoko wa M-Bet, Alan Mushi amesema wameridhia kuweka ‘Visit Tanzania’ kifuani kwakuwa wanajua umuhimu wa kutangaza Utalii na itakuwa faida kwa nchi nzima.

“Tunashukuru Wanasimba kwa kutupokea na kila kitu kinaenda sawa, sisi kama wadhamini wakuu tumeridhia kwa Simba kuwa na mdhamini mwingine kifuani ambao itakuwa ‘Visit Tanzania’,” amesema Mushi.

Mwakilishi kutoka Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Bernard Mtatiro ameushukuru Uongozi wa klabu kwa kuweka maslahi ya nchi mbele kwa kutangaza Utalii ambao umetoa ajira nyingi kwa Watanzania.

“Kwa niaba ya Bodi ya Utalii, nachukua nafasi hii kuishukuru Simba kwa jambo hili kubwa lenye maslahi mapama kwa nchi. Kitendo cha kuvaa jezi yenye jina la ‘Visit Tanzania’ katika michuano ya Afrika ambayo inaonyeshwa live itakuwa imetuongezea idadi kubwa ya Utalii,” amesema Mtatiro.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu, Imani Kajula amesema kila jambo ambalo Simba inalifanya kwanza tunaiweka Tanzania mbele kwa kila kitu.

“Leo wenye nchi tunaiweka nchi mbele kama, Kila tunachokifanya tunaiweka nchi mbele tumeamua kuitangaza nchi kupitia Utalii ambao unaliingizia taifa pato kubwa,” amesema Kajula.

Jezi zitaanza kuuzwa Februari 15 na bei yake itakuwa Sh. 35000.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER