Leo Tupo Jamhuri kuikabili Tanzania Prisons

Kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro kuikabili Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC ambao utaanza saa 10 jioni.

Tunaingia katika mchezo wa leo tukiwa tumetoka kufuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuifunga Jwaneng Galaxy mabao 6-0 wikiendi iliyopita.

Kikosi kipo kwenye hali nzuri na wachezaji wote wapo tayari na jana asubuhi wameshiriki mazoezi ya mwisho katika Uwanja wetu wa Mo Simba Arena tayari kwa mchezo wa leo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Daktari hakuna mchezaji yoyote ambaye amepata majeraha kwenye mazoezi ya mwisho ambayo yatamfanya kuukosa mchezo wa leo.

Matola atoa neno….

Kocha Msaidizi Seleman Matola amesema tunategemea kupata upinzani mkubwa na mchezo utakuwa mgumu lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda.

Matola amesema tunapokutana na Prisons mchezo unakuwa mgumu na amekiri kwa sasa ‘Wajelajela’ hao wapo kwenye kiwango bora lakini tumejipanga kuwakabili na lengo ni kuhakikisha tunapata pointi zote tatu.

“Tunategemea kupata upinzani mkubwa kutoka kwa Prisons, mara zote tunapokutana inakuwa mechi ngumu lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda,” amesema Matola.

Ni mechi ya kwanza ya nyumbani tukiwa Jamhuri……

Baada ya Uwanja wetu wa nyumbani wa Benjamin Mkapa kuwa kwenye ukarabati tutatumia Uwanja wa Jamhuri kwa mechi za nyumbani na leo itakuwa mechi yetu ya kwanza.

Kuanzia sasa mechi zetu zote za nyumbani tutacheza katika Uwanja wa Jamhuri tukianza na mechi ya leo.

Onana arejea……

Kiungo mshambuliaji Willy Onana amerejea kikosini baada ya kupona majeraha yaliyo muweka nje ya uwanja kwa takribani wiki tatu.

Onana jana amefanya mazoezi kikamilifu pamoja na wenzake  kama kocha Abdelhak Benchikha na wasaidizi wake wataona inafaa anaweza kumtumia kwenye mchezo wa leo.

Tuliwafunga 3-1 Sokoine

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya Oktoba 5 mwaka jana tulipata ushindi wa mabao 3-1.

Prisons walikuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na Edwin Balua kwa mpira wa adhabu uliotinga wavuni moja kwa moja huku mabao yetu yakifungwa na Clatous Chama, nahodha John Bocco na Said Ntibazonkiza kwa mkwaju wa penati.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER