Kazi ni moja tu Sokoine leo…

Kikosi chetu leo kitashuka katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya kwa kazi moja tu ya kuifunga Tanzania Prisons kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC utakaoanza saa 10 jioni.

Tunaingia kwenye mchezo wa leo tukiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi katika mechi zetu tatu mfululizo tangu turudi kwenye mapumziko ya kupisha mechi za kufuzu AFCON.

TUTAINGIA SOKOINE KWA UMAKINI MKUBWA

Kaimu Kocha Mkuu, Seleman Matola ameweka wazi kuwa tutaingia kwa tahadhari kwa kuwa tunajua alama tatu kwa wapinzani zitakuwa na faida kwao sababu hawapo kwenye nafasi nzuri.

Matola amesema mchezo utakuwa mgumu na tunaiheshimu Prisons na mara zote wamekuwa wakitupa upinzani mkubwa ingawa tumejipanga kuhakikisha tunashinda na kuchukua alama zote tatu.

“Tunajua mchezo utakuwa mgumu, mara zote tukikutana na Prisons mechi inakuwa ngumu hasa wakiwa Sokoine lakini safari hii itakuwa ngumu zaidi sababu hawapo kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo hivyo watataka kupata pointi tatu kutoka kwetu lakini tupo tayari kuwakabili,” amesema Matola.

BENO AWAITA MASHABIKI SOKOINE

Mlinda mlango Beno Kakolanya amewaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi kuja kuipa sapoti timu ili kujihakikishia kupata alama zote tatu ugenini.

“Kikubwa nawaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi kuja kutupa sapoti tunahitaji kushinda ili kuwapa furaha,” amesema Kakolanya.

BOCCO, MKUDE WAREJEA KIKOSINI

Nahodha John Bocco yupo kikosini baada ya kupona majeraha pamoja na kiungo mkabaji Jonas Mkude ambaye alikuwa nje ya uwanja muda mrefu.

TUTAWAKOSA SAKHO, KANOUTE

Katika mchezo wetu wa leo tutakosa huduma ya kiungo mshambuliaji Pape Sakho ambaye ameumia bega pamoja na Sadio Kanoute aliyekwenda nchini Mali kufuatilia hati yake ya kusafiria baada ya ile ya awali kuisha muda wake.

Pia tutaendelea kumkosa mlinda mlango Aishi Manula ambaye ana matatizo ya kifamilia.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER