Kocha Msaidizi wa Simba Queens, Mussa Hassan Mgosi amesema maandalizi ya mchezo wa kesho wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga Princess utakaopigwa saa 11 jioni katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Mgosi amesema timu imepata maandalizi ya kutosha kwa muda wa miezi miwili wamefanya mazoezi sasa wachezaji wapo tayari kwa mchezo huo na mingine inayofuata.
Mgosi amesema itakuwa mechi ngumu kwakuwa ni Derby na mara zote Simba na Yanga zikikutana mchezo unakuwa mgumu lakini kwa maandalizi waliyopata anaamini tutaibuka na ushindi.
“Timu iko tayari kwa ajili ya mchezo wa kesho, haitakuwa mechi rahisi na haijawahi kuwa rahisi kila tunapokutana na Yanga lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda,” amesema Mgosi.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji mlinzi, Violeth Nicholas amesema wapo kwenye hali nzuri kupambana kwa ajili ya kuipa timu matokeo.
“Kwa upande wetu wachezaji tupo tayari kuhakikisha tunapambana hadi mwisho kupata ushindi, tunawaheshimu Yanga na tunajua itakuwa mechi ngumu lakini tupo tayari,” amesema Violeth.