Karata ya kwanza ya Kombe la Shirikisho

Kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa saa 10 jioni kuikabili ASEC Mimosas katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Mchezo wa leo ni muhimu kwetu na tunahitaji kuhakikisha tunabaki na alama zote tatu katika uwanja wetu wa nyumbani.

Malengo yetu katika hatua hii ya makundi ni kuhakikisha tunapata alama tatu katika mechi zetu zote za nyumbani huku tukitafuta sare moja ili kujihakikishia kufuzu robo fainali.

KOCHA PABLO AFUNGUKA

Kocha Mkuu Pablo Franco amesema mchezo utakuwa mgumu na mzuri kutokana ubora wa wapinzani wetu lakini maandalizi tuliyofanya ukilinganisha na kutumia uwanja wa nyumbani anaamini tutaibuka na ushindi.

Pablo amesema changamoto ya kushindwa kutumia nafasi nyingi tunazotengeneza kwenye mechi zetu zilizopita imefanyiwa kazi mazoezini na tunarajia kupata mabao mengi kuanzia sasa.

“Ninaamini tutaanza kupata mabao mengi, tumekuwa tukifanya mazoezi kuhusu ufungaji na kila kitu kitakaa sawa kuanzia sasa.

“ASEC ni timu bora na ina uzoefu mkubwa katika michuano hii ya Afrika lakini tupo tayari kuhakikisha tunafanya vizuri katika uwanja wetu wa nyumbani,” amesema Pablo.

BOCCO AWAITA MASHABIKI KWA MKAPA

Nahodha John Bocco amewaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanjani ili kutoa sapoti kwa timu huku akiahidi kuwapa furaha.

Bocco amesema tutaingia katika mchezo wa leo bila kuwa na presha wala woga licha ya kukutana na timu bora yenye historia kubwa kwenye michuano ya Afrika.

“Tunaiheshimu ASEC ni timu bora na ina wachezaji wazuri lakini hatuigopi wala hatutaingia kwa presha. Tumejiandaa vizuri kimwili na kiakili kuhakikisha tunaibuka na ushindi.

“Kikubwa nawaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi uwanjani kuja kutupa sapoti, tunaamini tutawapa furaha kwa kupata ushindi,” amesema Bocco.

TULIVYOKUTANA MARA YA MWISHO

Agosti 24 mwaka 2003 tulikutana na ASEC katika mchezo wa makundi wa Ligi ya Mabingwa ambapo mechi ya mkondo wa kwanza iliyopigwa Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam tuliibuka na ushindi wa bao moja.

Mchezo wa marudiano uliopigwa nchini Ivory Coast tulipoteza kwa mabao 4-3 na kukosa nafasi ya kuingia nusu fainali.

SHARE :
Facebook
Twitter

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER