Kikosi chetu leo kitashuka katika Uwanja wa Jenerali Senyi Kountche kuikabili US Gendarmarie Nationale ya Niger katika mchezo wa kwanza ugenini wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Mchezo huo ni wa pili katika hatua ya makundi lakini ni wa kwanza ugenini baada ya ule tuliobuka na ushindi wa mabao 3-1 jijini Dar es Salaam dhidi ya ASEC Mimosas.
Kikosi kimewasili jana katika mji wa Niamey ambapo mchezo utapigwa na wachezaji wote waliosafiri wako tayari kwa mchezo.
Baada ya kuwasili kikosi kilifanya mazoezi ya mwisho ya kuwaweka wachezaji tayari katika Uwanja wa Jenerali Senyi Kountche.
PABLO ATAKA POINTI ZOTE TATU
Kocha Mkuu Pablo Franco pamoja na kukiri mchezo utakuwa mgumu lakini ameweka wazi tunahitaji kushinda na kupata alama zote tatu na endapo itashindikana basi tupate hata moja.
“Tutaingia katika mchezo wa leo kwa lengo la kutafuta pointi tatu muhimu ugenini, tusipofanikiwa tutahakikisha tunatafuta sare lakini si kupoteza.
“Tunajua mchezo utakuwa mgumu, Gendarmerie wametoka kupoteza mechi ya kwanza na watataka kutumia vema uwanja wa nyumbani lakini tumejipanga kuwakabili,” amesema Pablo
MANULA ATOA NENO
Mlinda mlango Aishi Manula amesema mchezo wa leo utatupa mwongozo wa tunachotarajia kukifanya kwenye mashindano hayo msimu huu.
“Huu ni mchezo wa pili ambao matokeo yake yatatupa mwongozo wa tunapoelekea. Tunaamini utakuwa mchezo mgumu lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda,” amesema Manula.
BANDA AAHIDI KUENDELEZA MOTO
Kwa upande wake Winga Peter Banda, amesema amejipanga kuwapa furaha mashabiki wetu kwa kuhakikisha anafanya vizuri kama ilivyokuwa katika mchezo dhidi ya ASEC Mimosas.
“Ndiyo malengo yangu kuhakikisha tunawapa furaha mashabiki wetu. Mimi ni mchezaji na natarajia kufanya vizuri kama ilivyokuwa mechi iliyopita,” amesema Banda.
MCHEZO KUANZA SAA MOJA USIKU
Mchezo wetu utaanza saa moja usiku kwa saa za nyumbani na saa 11 jioni kwa saa za Niger.