Gomez: Tulikuwa tayari kuwavaa Yanga

Kocha Mkuu Didier Gomez amesema kikosi chetu kilikuwa kwenye hali nzuri kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya watani wetu Yanga ambao umeahirishwa muda mfupi uliopita.

Mchezo huo umeahirishwa kutokana na mabadiliko ya ghafla ya muda wa kuanza kwa mechi ambayo awali ilipangwa iwe saa 11 jioni kabla ya kusogezwa hadi saa moja usiku hali iliyosababisha kutokea kwa sintofahamu.

Gomez amesema maandalizi yote ya mchezo yalikamilika na wachezaji walikuwa tayari kuelekea mchezo huo lakini hakuna namna kwani imeshatokea.

Raia huyo wa Ufaransa ameongeza kuwa alipenda kukutana na Yanga kabla ya kucheza mchezo wa robo fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Kaizer Chief ili kuongeza utimamu kwa wachezaji lakini imeshindikana hivyo tunajipanga kwa mechi ijayo.

“Wachezaji walikuwa tayari kwa ajili ya mchezo huu na maandalizi yalikuwa yamekamilika. Tulitamani tucheze mechi ya leo ili kuongeza utimamu kwa wachezaji lakini imeshindikana hivyo tunajiandaa kwa mchezo ujao,” amesema Kocha Gomez.

Gomez anaamini mkanganyiko uliotokea leo utamalizwa baada ya pande zote kukutana na kuzungumza huku akiwapa pole mashabiki waliojitokeza kwa wingi kutaka kushuhudia mtanange huo ambao haukufanyika.

“Tulipokea taarifa wote kuwa mchezo umesogezwa mbele, nawapa pole mashabiki wa Simba na wadau wa soka nchini kwa usumbufu ulijitokeza binafsi nimeshtushwa na hilo ila naamini litamalizwa salama,” amesema Gomez.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER