Mtendaji Mkuu wa Klabu, Imani Kajula ameishukuru Serikali kwa ukarabati mkubwa iliyofanya kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ambao tutautumia kwenye mchezo wa ufunguzi wa michuano ya African Football League (AFL) kwa kucheza na Al Ahly Oktoba 20.
Kajula amesema Uwanja wa Benjamin Mkapa umekarabatiwa vizuri na Serikali ingawa nasi tumechangia baadhi ya gharama.
Kajula amesema Oktoba 20 kutakuwa na viongozi mbalimbali kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF) pamoja na FIFA hivyo kila kitu kinaenda sawa.
Kajula ameongeza kuwa tunategemea mashabiki wengi watasafiri kutoka mikoani kuja kushuhudia mchezo hivyo jana tuliongeza na Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) ambao ni wabia wetu kupunguza bei ili watu wengi wajitokeze kwenye shughuli hiyo ya kihistoria.
“Tunaishukuru Serikali kwa ukarabati mkubwa iliyofanya kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ingawa na sisi pia tumechangia kidogo, Kiukweli sasa Uwanja unapendeza.
“Kutakuja viongozi wakubwa kutoka CAF na FIFA ndio maana tumetangaza viingilio mapema na Vituo vitakapopatikana ili kufanya zoezi la kuujaza uwanja wenye uwezo wa kujaza watu 60,000 liwe rahisi,” amesema Kajula.