Zoran: Wachezaji wote wako tayari kwa Geita Gold kesho

Kocha Mkuu Zoran Maki, amesema wachezaji wote wako kwenye hali nzuri kuelekea katika mchezo wetu wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Geita Gold utakaopigwa kesho katika Uwanja wa Benjamin Mkapa saa moja usiku.

Zoran amesema kikosi kipo kwenye hali nzuri hakuna majeruhi au mchezaji atakayekosekana kwa sababu yoyote kwenye mchezo huo.

Zoran ameongeza kuwa hatukupata muda wa kutosha kujiandaa na mchezo wa kesho baada ya kucheza Ngao ya Jamii Jumamosi na anaamini itakuwa mechi ngumu lakini tupo tayari kuwakabili Geita.

“Wachezaji wote wapo tayari kwa mchezo wa kesho, itakuwa jambo zuri kuanza kwa ushindi ingawa tunafahamu itakuwa mechi ngumu.

“Geita imemaliza nafasi ya nne msimu uliopita na sisi ya pili kwa hiyo inaonyesha zinakutakana timu mbili bora, ushindani utakuwa mkubwa lakini tumejipanga kwa ushindi,” amesema Kocha Zoran.

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji mlinzi wa kulia, Shomari Kapombe amesema wapo kwenye hali nzuri baada ya benchi la ufundi kuwaweka sawa kisaikolojia baada ya kupoteza Ngao ya Jamii na sasa wapo tayari kwa Geita.

“Kwanza tunashukuru kwa benchi la ufundi kutuweka sawa kisaikolojia, wamefanya kazi kubwa na tunaamini tutafanya vizuri. Geita ni timu nzuri na imekuwa ikitupa upinzani mkubwa lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda,” amesema Kapombe.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER