Mkutano Mkuu wa Wanachama wa Klabu yetu umefanyika leo Novemba 21 katika Ukumbi wa Kimataifa wa mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo umehudhuriwa na zaidi ya wanachama 800 kutoka sehemu mbalimbali nchini wakiwamo viongozi wote wa Bodi ya Wakurugenzi na viongozi wa zamani wa klabu.
MGENI RASMI ATOA NENO
Mgeni rasmi katika mkutano wetu alikuwa Mbunge wa Ilala, Mussa Azan Zungu ambaye amewataka wanachama, wapenzi na mashabiki kuendelea kushikamana katika nyakati zote.
Zungu amesema Simba ni timu nzuri lakini haimaanishi itashinda mechi kila siku kuna siku itafungwa na ikitokea hivyo tusiwanyooshee vidole viongozi badala yake tuendelee kushikamana.
TRY AGAIN AAHIDI MAKUBWA
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu, Salim Abdallah ‘Try Again’ amewataka wanachama wapenzi na mashabiki kutokuwa na wasiwasi kwa kuwa tunaenda kupata mafanikio makubwa ikiwamo kutetea ubingwa wa ligi, Azam Sports Federation Cup na Kombe la Mapunduzi.
Try Again amesema hakuna kitu cha kutuzuia kushindwa kufikia malengo yetu tuliyojiwekea lakini amesisitiza umoja na mshikamano.
MANGUNGU AFUNGUKA
Mwenyekiti wa klabu, Murtaza Mangungu amesema timu inaendelea kujidhatiti kuweka mipango dhabiti ndani ya uwanja na si nje.
Mangungu amesema mipango yetu ni kuongeza wanachama kupitia matawi, uendelezaji wa Uwanja wetu wa Mo Simba Arena, kujenga ukuta, kujenga gym, mabwawa ya kuogelea ili kuwa kamili.
Amesema viongozi na Bodi ya Wakurugenzi ipo tayari kukosolewa na kupokea maoni kutoka kwa wanachama na mashabiki lakini iwe kistaarabu.
BARBARA: 2021 HAKUNA TUTAKACHOACHA
Naye Mtendaji Mkuu wa Klabu, Barbara Gonzalez amesema malengo yetu msimu huu ni kutetea ubingwa wa ligi kuu, Azam Sports Federation Cup, kuchukua ubingwa wa Kombe la Mapunduzi pamoja na kufika nusu fainali ya michuno ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Barbara ameongeza kuwa msimu uliopita tulifanikiwa kwa asilimia 95 ndani na nje ya uwanja. Ndani ya uwanja tulitwaa ubingwa wa ligi, Azam Sports, Ngao ya Jamii na kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Lakini nje ya uwanja tumepata wadhamini lukuki kama Azam TV, Africarriers, Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Vunjabei, Emirate Aluminium ACP, Mo Extra na Mo 29 na wadhamini SportPesa ambao mkataba wao unaelekea ukingoni na mazungumzo kuongeza yanaendelea.
MO RAIS WA HESHIMA
Baada ya kujitoa kwa ajili ya klabu na kufanya uwekezaji mkubwa ndani ya klabu, Bodi ya Wakurugenzi kwa mujibu wa Ibara ya 51 imemteua Mohamed Dewji ‘Mo’ kuwa Rais wa heshima.