Kundi la kwanza la wachezaji 12 limefanyiwa vipimo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili ya kuangalia afya zao (check up) kabla ya kuanza Msimu wa Ligi 2023/24.
Zoezi hili litaendelea tena kesho kwa kundi la pili kufanyiwa vipimo kuashiria taa ya kijani kuelekea maandalizi ya msimu mpya wa ligi.
Daktari wa Timu, Edwin Kagabo amesema zoezi limekwenda vizuri na hali za wachezaji ziko vizuri ambapo wamepimwa vipimo vyote vya msingi ambavyo wanapaswa kuangaliwa.
“Tumewapima wachezaji wetu vitu muhimu vinavyohitajika kwa mchezaji kama uzito wa mwili, wingi wa damu, ufanyaji kazi wa figo na ini, wamefanyiwa mionzi (X-ray) ufanyaji kazi wa umeme kwenye moyo ili tufahamu utimamu wao kabla ya kuanza msimu,” amesema Dk. Kagabo.
Miongoni mwa wachezaji waliofanyiwa vipimo leo ni Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’, Mzamiru Yassin, Shomari Kapombe, Israel Patrick na Kibu Denis.
Asilimia kubwa wa wachezaji waliopimwa afya leo na watakaopimwa kesho ni wale wazamani huku wachezaji wapya waliosajiliwa wakirajiwa kufanyiwa vipimo punde tuu baada ya kuwasili
Huu ni utaratibu wetu kabla ya kuanza maandalizi ya msimu lazima tuwafanyie vipimo wachezaji ili kujua hali za afya zao kufuatia kutoka mapumzikoni.