Vitani kutupa karata yetu ya kwanza Angola leo

Kikosi chetu leo kitashuka katika Uwanja wa Novemba 11 saa 12 jioni kuikabili Premiero De Agosto katika mchezo wa hatua ya kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika.

Tutaingia katika mchezo wa leo tukifahamu hautakuwa rahisi na tutapambana kuanzia mwanzo hadi mwisho kuhakikisha tunapata matokeo mazuri.

MGUNDA: TUMEWAONA DE AGOSTO

Kocha Mkuu Juma Mgunda ameweka wazi kuwa tumewafuatilia wapinzani wetu De Agosto na tumeuona ubora wao na mapungufu yao ambayo tutayatumia kuhakikisha tunapata matokeo mazuri.

Mgunda amesema baada ya kuwaona wapinzani wetu tumeyafanyia kazi mapungufu mazoezini na tunaamini Mungu atakuwa upande wetu na wachezaji watafuata maelekezo waliyopewa.

“Tunajua tunacheza ugenini, utakuwa mchezo mgumu kwa kuwa wenzetu watakuwa na faida ya mashabiki lakini tumewaona na tutatumia mapungufu yao kuwadhuru na kujikinga na ubora wao,” amesema Mgunda.

BOCCO AFUNGUKA

Nahodha wa timu John Bocco amesema ingawa tuna uzoefu mzuri kwenye michuano hii lakini hatutawadharau wapinzani wetu badala yake tutapambana kuhakikisha tunafanya vizuri ugenini.

“Maandalizi yamekamilika, walimu wetu wamejitahidi kutuelekeza kitu ambacho tunapaswa kwenda kukifanya nasi wachezaji tupo tayari kukitekeleza uwanjani. Tumewasoma wapinzani wetu na tunajua pia nao wametusoma.

“Haitakuwa mechi rahisi ukizingatia kila timu iliyofika nafasi hii huwezi kuibeza, tutacheza kwa tahadhari zote ili mchezo wetu wa marudiano nyumbani tuwe kwenye mazingira mazuri ya kufuzu hatua ya makundi,” amesema Bocco.

MANULA ATOA NENO

Mlinda mlango Aishi Manula amesema benchi la ufundi limemaliza kazi yake kilichobaki ni kwao kama wachezaji kufuata maelekezo watakayopewa na walimu.

Manula ameongeza kuwa tunajua umuhimu wa michuano hii, malengo ya klabu pamoja na furaha ya Wanasimba hivyo tutahakikisha tunafanya kila linalowezekana kufanya vizuri ugenini.

“Kwa upande wetu wachezaji tupo tayari kuhakikisha tunapambana muda wote kushinda ili kutimiza malengo ya klabu na kuwapa furaha Wanasimba,” amesema Manula.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER