Kikosi chetu leo saa 10 jioni kitashuka katika Uwanja wa Uhuru kuikabili Namungo FC kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC.
Mara zote tunapokutana na Namungo mchezo unakuwa mgumu na wanatupa ushindani mkubwa lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda.
Tunaingia katika mchezo wa leo tukiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya watani.
Maandalizi ya mchezo yamekamilika…..
Kaimu Kocha Mkuu, Daniel Cadena amesema maandalizi ya mchezo yamekamilika na wachezaji wapo kwenye hali nzuri kuzipigania alama tatu.
Cadena amesema morali za wachezaji zipo juu na kila mmoja yupo tayari kucheza kama atapata nafasi.
“Tumewaandaa vizuri wachezaji kwa ajili ya mchezo wa kesho dhidi ya Namungo, tunawaheshimu wapinzani, na tumewafutailia. Tunategemea mchezo mgumu lakini tupo tumejipanga kupata ushindi,” amesema Cadena.
Bocco awaita mashabiki Uhuru……
Nahodha wa timu, John Bocco amewaomba mashabiki kuendelea kuipa sapoti timu bila kuangalia matokeo ya nyuma na wao kama wachezaji watahakikisha wanapambana ndani ya dakika 90 dhidi ya Namungo na kuwapa furaha.
“Hatuangalii yaliyopita, tunajipanga kwa kilicho mbele yetu. Ligi bado mbichi kikubwa tunaomba sapoti kutoka kwa mashabiki wetu tunaamini tutarudi kwenye ubora wetu,” amesema Bocco.
Tuliwafunga mchezo wa nyumbani…
Msimu uliopita tulifanikiwa kuwafunga bao moja nyumbani katika mchezo wa ligi uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Novemba 16.