Kikosi chetu kesho saa moja usiku kitashuka katika Uwanja wa CCM Mkwakwani kuikabili Singida Fountain Gate FC katika mchezo wa pili wa Ngao ya Jamii.
Hii ni mara ya kwanza mchezo wa Ngao ya Jamii kuhusisha timu nne na kupigwa nje ya jiji la Dar es Salaam.
Tayari kikosi chetu kimewasili jijini Tanga usiku wa kuamkia leo kikiwa na wachezaji wote tuliowasajili isipokuwa mlinda mlango namba moja Aishi Manula ambaye hali yake ya majeraha inazidi kuimarika.
Kikosi kipo tayari.
Leo jioni kikosi kitafanya mazoezi ya mwisho kujiandaa na mchezo wa kesho ambao tunaamini utakuwa mgumu kutokana na ubora wa wapinzani.
Baada ya Simba Day Nyota wapya kuonekana tena Tanga.
Msimu huu Ngao ya Jamii imekuwa mashindano sio kama ilivyokuwa miaka ya nyuma. Safari hii kutakuwa na nusu fainali na baadae fainali ambayo itapigwa Jumapili.
Nyota wetu ambao tumewasajili kwa ajili ya msimu huu wameonekana katika mchezo wa Simba Day tuliocheza dhidi ya Power Dynamos Agosti 6, na kesho wataonekana tena CCM Mkwakwani.
Tumesajili wachezaji wapya 10 kuelekea msimu mpya wa mashindano 2023/24 ambao Willy Onana, Aubin Kramo, Che Fondoh Malone, Abdallah Hamis, Shaban Chilunda, Hussein Kazi, David Kameta, Luis MiquissoneM Fabrice Ngoma na mlinda mlango, Hussein Abeli.
Chama kuikosa Singida kesho.
Kiungo mshambuliaji, Clatous Chama ataukosa mchezo wa kesho kutokana na kutumikia adhabu ya kufungiwa mechi tatu aliyopata mwishoni mwa msimu uliopita.
Tayari Chama amekosa mechi mbili za kumalizia msimu uliopita hivyo kesho anamaliza adhabu yake hivyo kama tukifanikiwa kutinga fainali ataruhusiwa kushiriki.