Tupo tayari kwa Derby ya Mzizima

Kikosi chetu leo kitashuka katika Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam, saa moja usiku kuikabili Azam FC (Derby ya Mzizima) katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC.

Mara zote tunapokutana na Azam mchezo huwa mgumu na hii inatokana na ubora wa timu unaochangiwa na mbinu za makocha.

Licha ya timu kuwa katika hali gani kwa kipindi hicho lakini tunapokutana mchezo unakuwa na ushindani mkubwa.

PABLO ATOA NENO

Kocha Mkuu Pablo Franco amesema mchezo utakuwa mgumu na tunatarajia kupata upinzani mkubwa mkubwa kutoka kwa Azam lakini tupo tayari kuwakabili.

Pablo amesema wachezaji wapo katika hali nzuri morali ipo juu na kila mmoja amejitahidi kuonyesha jitihada mazoezini ili apewe nafasi leo.

Pablo ameongeza kuwa tulikuwa na idadi kubwa ya wachezaji majeruhi lakini jambo jema ni kwamba baadhi yao wamerejea kikosini na wapo tayari kwa mchezo wa leo.

TUMEKUTANA MARA MBILI MSIMU HUU

Kabla ya mchezo wa leo tumekutana na Azam katika michezo miwili na yote tumefanikiwa kuibuka na ushindi.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa ligi uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Januari Mosi tuliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Tulikutana pia katika mchezo wa Fainali ya Kombe la Mapinduzi uliofanyika Uwanja wa Amani visiwani ZanzibarJanuari 13 tukaibuka na ushindi wa bao moja.

WATATU KUIKOSA AZAM LEO

Katika mchezo wa leo tutakosa huduma ya wachezaji wetu watatu ambao wanasumbuliwa na majeraha.

Nyota hao ni Clatous Chama na Jonas Mkude ambao hali zao zinaendelea vizuri na wanataraji kurejea uwanjani siku chache zijazo pamoja na Hassan Dilunga aliyefanyiwa upasuaji.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER