Kikosi chetu kiko tayari kwa ajili ya mchezo wa watani wa jadi Yanga utakaofanyika Jumamosi Julai 3, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa saa 11 jioni.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano, Haji Manara amesema maandalizi yanaendelea vizuri na wachezaji wapo kwenye hali na tayari kwa mtanange na afya zao ziko sawa.
Manara amesema kama waamuzi watakaopangwa kuchezesha watafuata sheria 17 za soka tutaibuka na ushindi wa mabao kuanzia matatu kutokana na ubora wa kikosi chetu.
Manara amewataja nyota wa kama Clatous Chama, Luis Miquissone, Rally Bwalya, John Bocco, Taddeo Lwanga na wengine kuwa wanaweza kufanya lolote kwenye mchezo na ndicho kinachotupa matumaini ya kuibuka na ushindi.
“Kikosi kipo tayari kwa mchezo, wachezaji wapo kwenye hali nzuri na hakuna mchezaji ambaye atakosa kutokana na majeruhi labda Jonas Mkude ambaye suala lake la kinidhamu halijakamilika,” amesema Manara.
Manara amewataka mashabiki wetu kujitokeza kwa wingi kuja kuishangilia timu kwa kuwa ndiyo siku ambayo tutawazwa Mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom kwa mara ya nne mfululizo.
“Nawaomba mashabiki wetu mjitokeze kwa wingi tena mje na makoti na suti kwa ajili ya kusherehekea ubingwa na tunawaomba TFF kama itawezekana watuletee kombe letu uwanjani,” amesema Manara.