Tupo tayari kumaliza kazi tuliyoianza Dar

Kikosi chetu leo kitashuka katika Uwanja wa Orlando nchini Afrika Kusini kuikabili Orlando Pirates katika mchezo wa marudiano wa Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ambao utaanza saa moja usiku kwa saa za nyumbani.

Tutaingia katika mchezo wa leo tukiwa na faida ya bao moja tulilopata katika mchezo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam Aprili 17, hivyo sare ya aina yoyote itatuvusha.

Tunafahamu mchezo utakuwa mgumu kutokana na ubora wa wapinzani lakini tumejipanga kuhakikisha tunapata matokeo mazuri na kutinga nusu fainali.

PABLO AKUMBUSHIA YA MWAKA 1993

Kocha Mkuu Pablo Franco amesema tangu mwaka 1993 tulipocheza fainali ya michuano hii hatujafika tena hatua hiyo kwa hiyo kipindi hiki tunapaswa kuivunja rekodi hiyo.

Pablo amesema Wanasimba na Watanzania kwa ujumla wanatamani kutuona tukivuka nusu fainali kitu ambacho tumejipanga kwa kila hali kuhakikisha tunafikia malengo hayo.

“Imepita miaka 29 tangu tulipocheza fainali ya michuano hii. Watanzania wanatamani kuiona timu yao ikifika hatua hii na tumejipanga kuhakikisha tunapita kwa kuitoa Orlando,” amesema Pablo.

MO AWAKUMBUSHA WACHEZAJI DHARAU ZA ORLANDO

Rais wa Heshima wa Klabu, Mohamed Dewji ‘Mo’ ameongea na wachezaji kwa njia ya video huku akiwambusha maneno ya kejeli yaliyotolewa na kocha wa Orlando baada ya mchezo wa kwanza hivyo tunapaswa kumfunga mdomo kwa kuwatupa nje ya mashindano katika ardhi yao ya nyumbani.

Mo amesema Orlando wametudharau kwa kuona hatukustahili kuwafunga hivyo tunapaswa kuongeza jitihada kwenye mchezo wa leo na kuwaduwaza wakiwa nyumbani kwao.

“Mimi naamini tunaweza kutinga nusu fainali. Tunapaswa kuwaonyesha kuwa tulistahili kuwafunga na tunawatoa katika ardhi yao ya nyumbani. Tuliwahi kufanya hivyo kwa Zamalek mwaka 2003 wengi hawakutegemea lakini ilitokea,” amesema Mo.

BWALYA: TUPO TAYARI KWA MAPAMBANO

Kiungo mshambuliaji Rally Bwalya, amesema kwa upande wao wachezaji wapo tayari wamepokea maelekezo kutoka benchi la ufundi mazoezini pamoja na nasaha kutoka kwa viongozi na kazi yao ni moja kufanya vitendo uwanjani.

“Sisi wachezaji tupo tayari kwa mchezo, tumepokea mafunzo ya kutosha kutoka kwa walimu. Tunajua mchezo utakuwa mgumu lakini tutapambana hadi mwisho ili kufuzu nusu fainali,” amesema Bwalya.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER