Leo saa 10 jioni kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa KMC Complex kuikabili Fountain Gate FC katika muendelezo wa Ligi Kuu ya NBC.
Tunaingia katika mchezo wa leo tukiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi mnono wa mabao 3-0 tuliopata katika mechi iliyopita dhidi ya Tabora United.
Tunafahamu utakuwa mchezo mgumu kutokana na ubora walionao Fountain Gate lakini tupo tayari kuwakabili.
Kocha Fadlu azungumzia mchezo wa leo.
Kocha Mkuu, Fadlu Davids amesema maandalizi ya mchezo yamekamilika na wachezaji wapo kwenye hali nzuri na matumaini ya kufanya vizuri ni makubwa.
Kocha Fadlu amesema kikosi chetu kinaendelea kupata muunganiko mzuri na sasa timu inatengeneza nafasi kuanzia nyuma katika idara ya ulinzi mpaka ushambuliaji.
“Malengo yetu ni kufanya vizuri katika kila mchezo, tunajua haitakuwa mechi rahisi lakini kikosi changu kipo tayari na jambo chanya ni kuwa tunaziedi kuimarika,” amesema Kocha Fadlu.
Wachezaji wapo tayari.
Kwa upande wake nahodha wa timu, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ amesema kwa upande wao kama wachezaji wapo tayari kufuata maelekezo ya walimu ili kuisaidia timu kupata matokeo chanya.
“Tunafahamu utakuwa mchezo mgumu, Fountain Gate wana timu imara lakini tumejipanga na tupo tayari kuwakabili na tutafuata maelekezo tutakayopewa na walimu wetu,” amesema Zimbwe Jr.
Mutale kuikosa Fountain Gate.
Kiungo mshambuliaji Joshua Mutale hatakuwa sehemu ya kikosi cha leo kutokana na kuendelea kuuguza jeraha la nyama za paja alilopata katika mchezo uliopita dhidi ya Tabora.
Taarifa rasmi zilizotolewa na Daktari wa timu, Edwin Kagabo nikuwa Mutale atakuwa nje ya uwanja kwa wiki mbili.