Leo saa 10 jioni kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kuikabili KMC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC.
Tutaingia katika mchezo wa leo tukiwa na kumbukumbu chanya ya mabao 4-1 tuliopata katika mchezo wa mwisho tuliocheza dhidi ya Geita Gold.
Tunahitaji kupata pointi tatu katika mchezo wa leo malengo yetu ni kuhakikisha tunamaliza katika nafasi mbili za juu kwenye msimamo wa Ligi.
Alichosema Kocha Mgunda …..
Kaimu Kocha Mkuu, Juma Mgunda amesema kikosi kipo kwenye hali nzuri kuelekea kwenye mtanange huo na tunategemea kupata upinzani mkubwa kutoka kwa KMC.
Mgunda ameongeza kuwa KMC ni timu bora na mara zote imekuwa ikitupa ushindani mkubwa lakini tumejipanga vya kutosha ili kupata ushindi.
“Maandalizi ya mchezo yamekamilika, wachezaji wangu wapo kwenye hali nzuri tayari kwa ajili ya mechi ngumu dhidi ya KMC,” amesema Mgunda.
Ally Salim aongea kwa niaba ya wachezaji….
Mlinda mlango, Ally Salim amesema wachezaji wote wapo tayari kwa ajili ya mchezo wa leo na lengo la kila mmoja ni kuhakikisha anaisaidia timu kupata matokeo chanya.
“Sisi kama wachezaji tupo tayari kwa mchezo, tunafahamu utakuwa mgumu. Tunaiheshimu KMC lakini tupo hapa kupambana hadi mwisho ili tupate pointi tatu,” amesema Ally Salim.
Chama, Miqussone ndani……
Viungo washambuliaji Clatous Chama na Luis Miqussone wapo tayari kwa ajili ya mchezo wa leo baada ya kupona majeraha yaliyokuwa yanawasumbua.
Nyota hao wamekosa mechi kadhaa lakini sasa wako kamili kushuka dimbani kuisaidia timu.
Jobe kuikosa KMC ………
Mshambuliaji Pa Omar Jobe hatakuwa sehemu ya mchezo wa leo kutokana na kupata maumivu katika mechi iliyopita dhidi ya Geita.
Kibu aanza mazoezi…..
Kiungo mshambuliaji Kibu Denis amerejea mazoezini baada ya kupona majeraha yaliyomuweka nje ya uwanja kwa muda mrefu.
Tulitoka sare tulipokutana mara ya mwisho…….
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Azam Complex Disemba 23 mwaka jana tulitoka sare ya kufungana mabao 2-2.