Tupo nyumbani kwa Mkapa kuikabili Ihefu leo

Kikosi chetu leo saa moja usiku kitashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Ihefu FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC.

Tunashuka katika mchezo wa leo tukiwa na lengo moja tu la kupambana kutafuta alama tatu muhimu ambazo zitatufanya kurejea nafasi ya juu kwenye msimamo.

Ingawa Ihefu haipo kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo kwa sasa lakini hilo halitupi kiburi cha kuamini tutapata ushindi kirahisi badala yake tutawaheshimu ili kutimiza malengo yetu.

MGUNDA AFUNGUKA

Kocha Mkuu Juma Mgunda, ameweka wazi kuwa msimu huu ligi ni ngumu na kila timu bila kujalisha ipo kwenye nafasi gani imejiandaa vizuri kupigania pointi tatu.

Mgunda amesema Ihefu ipo nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa ligi lakini tunajua mchezo wa leo utakuwa mgumu na watatupa upinzani mkubwa japokuwa tumejidhatiti kupata ushindi.

“Maandalizi yamekamilika kikosi kipo tayari kwa mchezo wa leo, tutaingia kupambana na Ihefu bila kutazama nafasi waliyopo. Tunaiheshimu Ihefu na tunaamini watatupa upinzani mkubwa,” amesema Mgunda.

ZIMBWE JR: TUKO TAYARI ASILIMIA 100

Nahodha Msaidizi Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ amesema wachezaji wapo tayari kwa ajili ya mchezo wa leo na maandalizi yamefanyika kwa ukamilifu.

Zimbwe amesema ushindi kwenye mchezo wa leo utatusaidia kupunguza tofauti iliyopo baina yetu na wanaongoza na kuzidi kuwapa presha.

“Sisi wachezaji tupo tayari kwa mchezo, tunajua utakuwa mgumu. Tumetoka kucheza mechi ngumu dhidi ya Singida na hatujapata matokeo mazuri kwa hiyo tutajitahidi kupata ushindi leo,” amesema Zimbwe Jr.

HALI YA KIKOSI

Kocha Juma Mgunda amewataja Peter Banda, Jimmyson Mwanuke na Israel Patrick kuwa ndiyo wachezaji majeruhi ambao hawatakuwa sehemu ya mchezo wa leo.

Kiungo Clatous Chama nae anaendelea kutumikia adhabu ya kufungiwa mechi tatu hivyo hatakuwa sehemu ya mchezo wa leo pia.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER