Tupo kwa Mkapa tena kuikabili Ruvu Shooting Leo

Kikosi chetu leo kitashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa saa moja usiku kuikabili Ruvu Shooting kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC.

Tunaingia katika mchezo wa leo tukiwa tunajua tunakutana na timu imara yenye wachezaji bora pamoja na benchi bora la ufundi lakini tumejipanga vizuri kuhakikisha tunapata ushindi.

Wachezaji wamefanya mazoezi ya mwisho katika Uwanja wa Mo Simba Arena na wapo kwenye hali nzuri tayari kupambana kupata alama tatu muhimu kwenye mchezo wa leo.

ALICHOSEMA KOCHA MGUNDA

Kocha mkuu, Juma Mgunda amesema mchezo utakuwa mgumu kutokana na ubora wa wapinzani Ruvu Shooting wakiongozwa na benchi la ufundi chini ya kocha Charles Boniface Mkwasa.

Mgunda amesema maandalizi ya mchezo yamekamilika na wachezaji wapo kwenye hali nzuri tayari kupigania pointi tatu muhimu.

“Tunaiheshimu Ruvu, ni timu nzuri na ina kocha mwenye uzoefu lakini tumefanya maandalizi mazuri na tupo tayari kwa mchezo lengo likiwa ni kutafuta pointi tatu,” amesema Mgunda.

ALLY SALIM: TUPO TAYARI KWA MCHEZO

Mlinda mlango, Ally Salim amesema kwa upande wao wachezaji wapo kwenye hali nzuri na tayari kufuata maelekezo watakayopewa na benchi la ufundi.

Salim amesema ushindi kwenye mchezo wa leo ndio jambo pekee ambalo wataingia uwanjani kulipigania kwakuwa kila mechi ni fainali kutokana na ugumu wa ligi.

“Sisi wachezaji tupo tayari, maandalizi yamekamilika na maelekezo tuliyopewa na benchi letu la ufundi tutahakikisha tunayafuata ili kupata pointi tatu muhimu,” amesema Ally.

CHAMA AREJEA MZIGONI

Kiungo mshambuliaji, Clatous Chama amerejea kikosini baada ya kumaliza adhabu ya kufungiwa mechi tatu na kocha Mgunda ameweka wazi atakuwa sehemu ya mchezo wa leo.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER