Tupo kwa Mkapa leo kuikabili Dodoma Jiji

Kikosi chetu leo saa moja usiku kitashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Dodoma Jiji katika muendelezo wa Ligi Kuu ya NBC.

Mchezo wa leo utakuwa wa tano kwetu msimu huu tukishinda minne na kutoka sare mmoja ambapo tumejikusanyia alama 10.

Wachezaji wote wamefanya mazoezi ya mwisho jana katika Uwanja wetu wa Mo Arena na wapo katika hali nzuri tayari kwa mchezo wa leo.

MATOLA ATOA NENO

Kocha Msaidizi Seleman Matola ameweka wazi kuwa mchezo utakuwa mgumu licha ya Dodoma Jiji kutoanza vizuri msimu kutokana na matokeo waliopata.

Matola amesema mara zote kila timu inapokutana nasi inapambana kuonyesha uwezo ndyo maana tutaingia kwa tahadhari zote bila kuidharau Dodoma.

“Tumepata muda wa siku mbili kufanya mazoezi baada ya kurudi Zanzibar, tunajua utakuwa mchezo mgumu licha ya Dodoma kuanza vibaya ligi lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda,” amesema Matola.

ZIMBWE JR AWAITA MASHABIKI KWA MKAPA

Nahodha msaidizi Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ amewaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanjani ili kuwapa sapoti wachezaji na kuchagiza kupatikana kwa ushindi.

“Kama kawaida tunawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kuja kutuunga mkono nasi tupo tayari kuhakikisha tunawapa furaha,” amesema Zimbwe Jr.

KAPOMBE, BANDA, SAKHO NJE

Katika mchezo wa leo tutawakosa nyota wetu watatu Shomari Kapombe, Peter Banda na Pape Sakho.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER