Tupo kamili kwa Geita Gold

Kikosi chetu leo kitashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Geita Gold kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC utakaoanza saa moja usiku.

Tutaingia katika mchezo wa leo tukiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao 3-1 tuliyopata katika mechi iliyopita dhidi ya Ruvu Shooting.

Mchezo huo uliopigwa Uwanja wa CCM Kirumba ulikuwa wa kwanza kwa Kocha Pablo Franco ambapo timu ilionyesha kiwango safi cha kuvutia mbele ya mashabiki.

Kuelekea mchezo wa leo Kocha Msaidizi Seleman Matola amesema utakuwa mgumu na tutaingia kwa tahadhari zote ikiwemo kuwaheshimu wapinzani ili kuhakikisha tunachukua alama zote tatu.

Matola ameongeza kuwa hatutaidharau Geita kwa namna yoyote tutacheza kwa kujituma lengo likiwa kuendelea kuifukuzia nafasi ya kileleni mwa msimamo na kuwapa furaha Wanasimba.

“Geita si timu mbaya, ipo vizuri na tunaiheshimu. Tutaingia uwanjani tukiwa na tahadhari zote tunahitaji kupata alama zote tatu. Wachezaji wote wapo kambini tayari kwa mchezo,” amesema Matola.

MAANDALIZI YAMEKAMILIKA

Kuelekea mechi ya leo maandalizi yote yamekamilika wachezaji walipata siku mbili za kufanya mazoezi baada ya mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Red Arrows, Jumapili iliyopita.

Wachezaji wote wapo kambini na wamefanya mazoezi ya mwisho hivyo benchi la ufundi litakuwa na wigo mpana wa kuchagua kikosi kitakachoshuka uwanjani.

SHARE :
Facebook
Twitter

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER