Tupo kamili kutafuta pointi tatu Ilulu leo

Kikosi chetu leo kitashuka kwenye Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi kuikabili Namungo FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC ambao utaanza saa 10 jioni.

Wachezaji wote 23 waliosafiri jana wamefanya mazoezi ya mwisho na jambo jema ni kwamba hakuna aliyepata majeraha yatakayomfanya kuukosa mchezo.

Morali kwa wachezaji ipo juu na wapo tayari kuhakikisha tunapambana katika kila mchezo kupata pointi tatu ili kupunguza tofauti ya alama iliyopo na wanaoongoza.

PABLO AFUNGUKA

Kocha Mkuu Pablo Franco amesema mchezo wa leo utakuwa mgumu kwetu kutokana na kutopata muda wa kufanya maandalizi mazuri kwa sababu ya ratiba kutubana.

Pablo amesema tumetoka kucheza mechi kubwa ya Derby siku ya Jumamosi siku moja Jumatatu tumeanza safari na leo tunacheza hivyo wachezaji hawajapumzika vya kutosha wala kufanya mazoezi ipasavyo.

“Ukweli ni kwamba mchezo utakuwa mgumu sababu hatujafanya mazoezi ya kutosha, ratiba ni ngumu tunacheza mechi karibu karibu lakini sisi ni Simba tutapambana katika hali zote.

“Namungo ni timu nzuri nakumbuka tulicheza nayo kwenye michuano ya Mapinduzi, tuliwafunga lakini walitupa upinzani mkubwa. Naamini hata leo itakuwa hivyo,” amesema Pablo.

TUMEIFUNGA NAMUNGO MARA MBILI MSIMU HUU

Kabla ya mchezo wa leo tumekutana mara mbili na Namungo msimu huu, mechi ya mzunguko wa kwanza wa ligi na Nusu Fainali ya Michuano ya Mapinduzi tukiibuka na jumla ya mabao 3-0.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa Novemba 3, 2021 tuliibuka na ushindi wa bao moja lililofungwa na Medie Kagere.

Nusu Fainali ya Mapinduzi iliyopigwa Januari 10, 2022 Uwanja wa Amani Visiwani Zanzibar tuliibuka na ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa na Medie Kagere na Pape Sakho.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER